Saturday, January 2, 2016

Tatizo sio kutokuwa na pesa ila tatizo ni unazifanyia nini hizo pesa. Kutokuwa na pesa za kutosha si tatizo kabisa. Wengi husema kuwa hakuna mtu hutosheka na pesa na mara zote pesa huwa hazitoshelezi. Leo nakuambia kuwa jambo la msingi sio kutosheleza kwa pesa au uchache wake bali ni jinsi zinavyotumika.
Kuna dhana inaitwa "Nidhamu ya Pesa" Neno nidhamu wengi wamelizoea kwa kulisikia na kulitumia tangu utotoni lakini hawajui kuwa neno hilo lina maana zaidi ya ile tuliyoizoea. Nidhamu (Discipline) ya pesa ni dhana ambayo inajumuisha kila kitu kinachofanyika kwa kutumia pesa kama vile vyanzo vya pesa zako, malengo na matumizi ya hizo pesa.nk. Nidhamu ya pesa ndiyo itakayomfanya mtu kutoka kuwa masikini na kuwa tajiri. Kwa hivo ni nidhamu ya pesa inayotofautisha kati ya waliofanikiwa na wanaondendelea kudidimia au kujikongoja katika dimbwi la umasikini kwa kisingizio cha pesa hazitoshi. Je unataka kutoka hapo ulipo kuachana na hali uliyonayo na kuwa vile unataka uishi? Je, wewe pia unadhani pesa hazitoshi? Fuatilia makala hii na hakika utaona na kuthibitisha kuwa Tatizo sio kutokuwa na pesa..  Katika suala la nidhamu ya pesa kuna hatua saba kama ifuatavyo.
 
1. Zielewe Pesa Zako
 Hatua ya kwanza ni muhima na ni lazima sana wewe kuzielewa pesa zako. Nini maana yake? Kuzielewa pesa zako ni kufahamu 'ndani nje' (A-Z) kuhusu wapi unazipata, kiasi gani, wapi unazihifadhi na  nani anatumia pesa zako? Wapo wengine wanafahamu zaidi kuhusu pesa za wengine kuliko za kwao. Wanaweza kuzungumza kuhusu tajiri fulani jinsi anavyozitafuta pesa lakini hawajui na hawasemi chochote kuhusu wao wenyewe na pesa zao. Zielewe pesa zako, fahamu chanzo cha pesa zako kama ni mshahara kila mwezi, posho ya kila siku au kila wiki, biashara, marupurupu au msaada kutoka kwa marafiki na watu wako wa karibu. Ukijua vyanzo vyote vya pesa zako nenda mbele zaidi na utambua ni kiasi gani unapata katika vyanzo hivyo kwa ujumla wake.

2. Yafahamu Matumizi yako.
 Baada ya kujua kuhusu vyanzo vyako vya mapato lazima ujue matumizi yako na uyaweke katika makundi kulingana na umuhimu wake. Utajua matumizi yako baada ya kutafakari kwa undani kuhusu mahitaji yako kwa kipindi fulani (mfano, wiki moja au mwezi mmoja) kwa kuwa matumizi yanatokana na mahitaji. Yapo mahitaji ya lazima, (mfano kodi zote,chakula, ada..), mahitaji ya muhimu (mfano nguo), na mahitaji yasiyo ya muhimu, waweza kuyaita mahitaji haya viburudisho (mfano pombe). Katika kutumia pesa zako zitenge katika makundi kulingana na makundi kama tulivyotaja hapo juu. Kumbuka kuweka pesa zaidi kwa ajili ya mahitaji ya lazima (kwa kuwa yaweza kutokea dharura).


3. Weka Malengo
Waweza kuweka malengo kwa mfano lengo la kununua kiwanja, au kununua chochote kile ambacho kinahitaji pesa nyingi zaidi ya vyanzo vyako vya pesa. Weka malengo baada ya kujua ni kiasi gani unatumia kila mwezi katika mahitaji yako na kiasi gani unahifadhi ili kutimiza malengo yako. Punguza matumizi hasa yasiyo ya lazima na yale yasiyo ya muhimu. Ile pesa ambayo ungetumia katika vitu hivyo hifadhi kwa ajili ya malengo yako. Weka malengo na timiza malengo yako.


4. Hifadhi pesa kila unapozipata
 Kuhifadhi pesa ni baada ya kutambua mapato na matumizi yako (bajeti). Jikumbushe kila mara kutotumia pesa zako katika vitu vya starehe kama pombe au ofa kwa wengine ili uonekane. Epuka kutoa misaada isiyo ya lazima na andika bajeti (mapato na matumizi yako). Fahamu kwa undani kila pesa inayoingia na jinsi gani inatumika au kuhifadhiwa hata kama ni shilingi mia.

5. Matamanio
Weka  malengo ya muda ya kununua vile unavyovitamani au visivyo vya lazima (matamanio) kama vile simu mpya, pochi.....Kila siku ukitoka nyumbani beba pesa unazozihitaji tu na si zaidi ili uepukane na vishawishi vya kununua unavyovitamani.

6. Pesa usizozitarajia
Kuna wakati unapewa pesa ambazo hukuzitarajia mfano marupurupu, zawadi, nk. Zitumie pesa hizi kulipi mahitaji ya lazima au zihifadhi moja kwa moja kwa ajili ya matumizi ya baadaye.






7. Jipongeze
Kwanini au namna gani utajipongeza? Baada ya kujitahmini na kujua kuwa kwa kiasi fulani unaweza kuzimudu pesa zako, na umejua ya kuwa bajeti yako imekwenda namna ulivyopanga na malengo na matamanio yamweza kufikiwa jipongeze kwa kufanya matumizi kidogo. Fanya hatua hii baada ya kila muda fulani (mfano miezi sita) Nenda mahali pa utulivu (beach, au popote upapendapo) na upumzishe akili yako. Hii itakusaidia kupata nguvu ya kuendelea mbele zaidi na kuyafikia mafanikioa. 






0 comments:

Post a Comment

Popular Posts

Recent Posts

FOLLOW US